NDOA NI KAMA YAI

Hongera nawapatia, bwana na bibi harusi
Kwa kufunga yenu ndoa, nawalaki kwa kikosi
Msojua mtajua, msende mwendo wa kasi
Hino ndoa kama yai, chungeni isivundike

Nawatakia salama, yenu yawe ni ya kheri
Muishi maisha mema, msikutwe nayo shari
Mzae watoto wema, wenye kumcha Qahari
Hino ndoa kama yai, chungeni isivundike

Indhari tukueni, muihifadhi moyoni
Yanayojiri nyumbani, ni siri yenu ya ndani
Yasipekwe kawandani kuwatia izarani
Hino ndoa kama yai, chungeni isivundike

Pamoja mshikaneni, na wala msiatane
Mazuri ambianeni, na mabaya mkanyane
Vicheko pia chekeni, maliwazo mpeane
Hino ndoa kama yai, chungeni isivundike

Kamba kwa shime vuteni, karipieni uvivu
Umoja udumisheni, ndipo mtapata nguvu
Maisha ulimwenguni, yahitaji ushupavu
Hino ndoa kama yai, chungeni isivundike

Matatizo kutokea, silo jambo la ajabu
Hayo yatawafikia, ingawa si matulubu
Kuelewana ndo ndia, ya kuimaliza tabu
Hino ndoa kama yai, chungeni isivundike

Vidudu watu wa tele, waipendayo zahama
Kwenu watapija lele, kuanzisha hiyo ngoma
Ikishazuka kelele, haraka watayoyoma
Hino ndoa kama yai, chungeni isivundike

Yao msiyasikize, hiyo ni yao ibada
Na wala msiyawaze, kwani hayana faida
Wacha waipige zeze, mwisho watakosa rada
Hino ndoa kama yai, chungeni isivundike

Kwa Mola elekeeni, ibada muidumishe
Radhi yake iyombeni, mema kwenu afikishe
Awaingize peponi, na moto awaepushe
Hino ndoa kama yai, chungeni isivundike

Install Palscity app